Kampuni
ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania leo imetangaza kufanyika kwa
kliniki ya soka ya Kimataifa ya Manchester United hapa Dar es Salaam
kuanzania 23 -27 Aprili mwaka huu.
Mkurugenzi wa Mawasiliano
Airtel Tanzania Beatrice Singano akiongea na waandishi wa Habari wakati
wa kutangaza Kliniki ya Kimataifa ya mpira wa soka ya Manchester United
ambayo itafanyika Jijini Dar es Salaam April 23-27 chini ya wakufunzi
kutoka Klabu ya Manchester United. Kushoto ni Mkurugenzi wa Mashindano
ya Vijana Ayoub Nyenzi.
Kliniki
hiyo ambayo itafanyika kwenye uwanja wa Azama FC (Chamazi Complex
Stadium), ina nia ya kuwaendeleza vijana waliofanya vizuri kwenye
michuano ya mwaka jana ya kimataifa ambayo ilifanyika Lagos, Nigeria na
kushirikisha nchi 12 ambapo timu ya Tanzania ya wasichana iliibuka
mabingwa.
Hii
ni mara ya pili kwa kliniki kama hiyo kufanyika hapa nchini kufuatia
kliniki kama hii liyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa 2011. Kliniki
nyingine ilifanyika Nairobi 2012 na Tanzania iliwakilishwa na wavulana
watatu na wasichana watatu.
Kama
ilivyokuwa kwenye kliniki zilizopita, kliniki ya mwaka huu itaendeshwa
na makocha kutoka shule za soka za Klabu ya Manchester United na
wanatarajiwa kutoa mafunzo ya awali ya mpira wa miguu kama vile kupiga
pasi, kukimbia na mpira, kupiga mashoot, nidhamu na nyingine nyingi.
Akiongea
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa
Mawasiliano wa Airtel Tanzania Beatrice Singano alisema kliniki hiyo ni
sehemu ya mpango kapambe wa Airtel kusaka na kuendeleza vipaji vya soka
hapa Tanzania na Barani Afrika kwa ujumla.